DEVAN:   Proposal, Marketing, Communications & Events Management Services

Tanzania Women in Communication Forum 2026 yazindua historia mpya ya wanawake katika Tasnia ya Mawasiliano Tanzania

  • Home
  • News & Events
  • Tanzania Women in Communication Forum 2026 yazindua historia mpya ya wanawake katika Tasnia ya Mawasiliano Tanzania
blank

Katika zama ambazo simulizi zina uwezo wa kubadili mwelekeo wa taifa, Tanzania imeandika ukurasa mpya kupitia kufanyika kwa Tanzania Women in Communication Forum 2026; jukwaa la kihistoria lililowakutanisha wataalamu, wadau na viongozi wa mawasiliano kujadili nafasi ya mawasiliano ya kimkakati katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Kwa kaulimbiu yake “Give to Gain: Elevating Women in Communication, Public Relations and Media”, forum hii haikuwa tu mkutano wa kitaaluma bali ilikuwa ni mwamko wa pamoja wa kujenga kizazi cha wanawake wanaotumia mawasiliano kama nyenzo ya maendeleo jumuishi na endelevu.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Dkt. Blandina Kilama, Naibu Katibu Mtendaji; Biashara na Ubunifu, Tume ya Taifa ya Mipango, aliwasilisha salamu za Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais; Mipango na Uwekezaji, huku akisisitiza kuwa mawasiliano ni daraja muhimu linalounganisha sera, taasisi na wananchi katika safari ya kuelekea Dira 2050. Alieleza kuwa katika zama za mapinduzi ya kidijitali, wataalamu wa mawasiliano wanapaswa kuhakikisha taarifa sahihi, uwazi na uaminifu vinatawala ili kuimarisha ushirikishwaji wa wananchi katika maendeleo. Aidha, alitambua mchango wa wanawake kama mabalozi wa mabadiliko ya kijamii na kiuchumi, na kupongeza wazo la kuanzishwa kwa Tanzania Women in Communication Association (TWICA) kama jukwaa la kuimarisha mshikamano, ujuzi na ukuaji wa taaluma hiyo nchini.

blank

Akisisitiza zaidi, Dkt. Blandina alibainisha kuwa taaluma ya mawasiliano ni zaidi ya ajira; ni wajibu wa kujenga taifa. Alieleza kuwa sauti za wataalamu wa mawasiliano zina uwezo wa kuhamasisha kizazi kijacho, kuimarisha uwajibikaji, kuonesha mafanikio ya taifa na kujenga matumaini ya pamoja. Alitoa wito kwa washiriki kutumia jukwaa hilo kujifunza, kushirikiana na kujenga mitandao imara ya kitaaluma itakayochochea ukuaji wa sekta ya mawasiliano yenye weledi, maadili na mchango mkubwa katika maendeleo ya muda mrefu ya taifa..

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Devan PR & Event Management Bi. Salima Mseta ambao ni mwandaaji wa Jukwaa hili alieleza kuwa kuanzishwa kwa forum hii ni mwanzo wa safari ya kimkakati ya kujenga mtandao imara wa wanawake katika mawasiliano nchini. Alisisitiza dhamira ya kuifanya forum kuwa ya kila mwaka, huku lengo kuu likiwa kuanzisha rasmi TWICA,  chombo kitakachowaunganisha wanawake wataalamu wa mawasiliano, kukuza ushirikiano, kuimarisha uongozi, kuendeleza maadili ya taaluma na kutoa jukwaa la majadiliano ya kitaifa. Alibainisha kuwa TWICA inalenga kuwa nguvu ya pamoja itakayochochea mchango wa wanawake katika kusimulia hadithi za maendeleo ya taifa na kuunga mkono utekelezaji wa Dira 2050.

blank

Mijadala ya wataalamu(wawezeshaji) ilitoa mwanga mpana kuhusu mustakabali wa taaluma ya mawasiliano, ambapo wataalamu kutoka sekta mbalimbali walishirikisha uzoefu, changamoto na fursa zilizopo. Kwa upekee, mwakilishi kutoka TFF alitoa wito wa kuishirikisha TWICA katika maandalizi ya AFCON 2027, akisisitiza nafasi ya mawasiliano ya kimkakati katika kuijenga taswira ya taifa kimataifa na kuhakikisha mafanikio ya matukio makubwa ya kimataifa.

Forum hii imeacha alama isiyofutika kwa kuibua maono mapya ya ushirikiano, uwezeshaji na uongozi wa wanawake katika mawasiliano. Devan PR & Event Management, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wanatoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo kwa kuitikia mwaliko na kutuma uwakilishi wake, pamoja na washirika, wadhamini, wanatasnia, vyombo vya habari na washiriki wote walioonesha imani na kuwa sehemu ya historia hii.

blankblankblank

Kwa pamoja, Tanzania Women in Communication Forum 2026 imeweka msingi imara wa kuanzishwa kwa TWICA na kuthibitisha kuwa katika kusheherekea siku ya wanwake duniani chini ya “Give to Gain” si kauli mbiu tu, bali ni wito wa vitendo utakaokumbukwa daima katika kujenga mustakabali wa mawasiliano nchini Tanzania.

Je, wewe ni mtaalamu wa mawasiliano nchini Tanzania? Wasiliana nasi kupitia info@devanpragency.co.tz  au piga simu +255 778 626 022 ili kujiunga na jukwaa la wanawake katika tasnia ya mawasiliano kupitia WhatsApp Group. Pia, tufuatilie kupitia ukurasa wa @tzwomenincommunication na @devan_prandevents kwa taarifa na fursa zaidi.

blankblank

blankblankblank

Previous Post
Newer Post

Leave A Comment